Subscribe Us

Header Ads

Zaidi Ya Bilioni 460 Kufungua Mkoa Wa Kigoma Kwa Barabara Za Lami



Serikali imepanga kutumia zaidi ya shilingi Bilioni 460 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami ili kuweza kuufungua kibiashara na kuchochea fursa nyingi za kimaendeleo katika mkoa wa Kigoma.

Aidha, Bilioni 21 zimetolewa kwa ajili ya miradi mingine ya nyongeza ambayo itagusa jamii inayozunguka katika miradi ikiwemo ujenzi wa wa Shule, Soko, Miundombinu ya Maji Safi na Taka na Vituo cha Mabasi katika wilaya za Buhigwe, Kasulu na Kibondo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Godfrey Kasekenya, wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Manyovu mara baada ya kukagua hatua ya ujenzi wa barabara ya Kanyani – Kidyama – Mvugwe (km 70.5), Njia panda ya Kasulu – Manyovu (km 68.25) pamoja na eneo patakapojengwa Kituo cha Kisasa cha Pamoja cha Manyovu/Mugina (OSBP) mpakani mwa Tanzania na Burundi.

Naibu Waziri huyo amezitaja barabara ambazo zinatekelezwa kwa fedha hizo ikiwa ni ujenzi wa barabara ya Njia panda ya Nduta – Kabingo (km 62.5), Njiapanda ya Nduta – Kibondo Mjini (km 25.9), Mvugwe – Njiapanda ya Nduta (km 59.35), Kanyani – Kidyama – Mvugwe (km 70.5), Njia panda ya Kasulu – Manyovu (km 68.25) ambazo zinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba, 2023.

“Serikali imeamua kuweka wakandarasi wengi katika mkoa huu kwa kuwa Kigoma haukuwa umefunguka kwa barabara za lami sasa zimeanza kujengwa hivyo tunawajibu kama wananchi kulinda miundombinu hii na kujiweka tayari kwa kufanya biashara na mikoa mingine ya jirani ili kujiongezea kipato”, amefafanua Kasekenya.

Ameongeza kuwa tayari wakandarasi wapo eneo la kazi kutokea Kigoma ukielekea Tabora kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Uvinza – Malagarasi (km 51.1) na Kazilambwa – Chagu (km 36) kwa kiwango cha lami.

Katika kufungua mkoa wa Kigoma na Katavi, Eng. Kasekenya amesema kuwa tayari mkandarasi amekwishaanza ujenzi kutokea Mpanda (km 50) kuelekea Uvinza ili kupunguza umbali wa safari ukitokea Katavi.