KESI ya mauaji inayomkabili mke wa aliyekuwa bilionea wa madini, marehemu Erasto Msuya, Miriam Mrita na mwenzake itaendelea kusikilizwa leo baada ya kuahirishwa kwa siku tano.
Mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni mfanyabiashara, Revocatus Muyella. Machi 2 mwaka huu Jaji Edwin Kakolaki aliahirisha kesi hiyo baada ya shahidi wa tano, Latifa Mohammed kumaliza kutoa ushahidi na upande wa mashitaka ukadai kuwa hawakuwa na shahidi mwingine hivyo wakaomba muda wa kuwaandaa mashahidi wengine.
Jaji Kakolaki aliarisha kesi hiyo hadi leo wakati shahidi wa sita atakapoanza kutoa ushahidi. Awali shahidi wa kwanza, Inspekta Mwajuma aliomba kuwasilisha maelezo ya onyo ya Mrita mahakamani. Ombi hilo lilipingwa kwa madai kuwa Mrita aliteswa na kusainishwa hati ya kiapo bila kujua kilichomo ndani ya maelezo ya onyo.
Hali hiyo ilizua mjadala wa kisheria na kusababisha kufunguliwa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi ili kuthibitisha hoja hizo. Baada ya kusikilizwa pande zote mbili katika kesi hiyo ndogo, Jaji Kakolaki aliona hoja za upande wa utetezi hazina mashiko na hivyo kutupilia mbali pingamizi lao na kuendelea na ushahidi katika kesi ya msingi.
Hadi sasa mashahidi watano wametoa ushahidi akiwemo Hakimu mstaafu, Leonia Mutta ambaye alisikiliza Maungamo ya Mrita akiwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala na mlinzi wa amani aliyesikiliza maungamo ya mshitakiwa huyo.
Mashahidi hao walidai kuwa mshitakiwa huyo alikiri kuhusika na mauaji hayo na Ofisa wa Polisi, Latifa Mohamed alidai kuwa mahojiano aliyofanya na Mrita yalikuwa yamerekodiwa katika mfumo wa video.
Jirani wa marehemu Aneth, Mwanaisha Kassim ambaye ni shahidi wa tatu wa upande wa mashitaka alieleza namna alivyofuatwa na mtoto wa marehemu na baadaye kwenda nyumbani kwa marehemu na kukuta mwili wake ukiwa utupu na kufunikwa kitambaa usoni.
Shahidi mwingine, SSP Richard Mwaiseba alieleza namna alivyoukuta mwili wa marehemu chumbani kukiwa na kisu chini ya sofa lililokuwa humo chumbani na pia akaeleza namna yeye na timu ya uchunguzi walivyochunguza na baadaye kuondoka kabla ya mwili kwenda kuhifadhiwa.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Mrita kwa kushirikiana na mtu aliyemtaja kwa jina la Ray walitumia siku 10 kupanga mipango ya kutekeleza mauaji ya Aneth na waliamua Aneth Mei 25, 2016 nyumbani kwa marehemu Kibada, Kigamboni Mkoa wa Dar es Salaam.