BODI ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) imewafutia usajili wakandarasi zaidi ya 4,000 kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ubabaishaji kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi.
Msajili wa CRB, Rhoben Nkori amesema hatua ya kuwafutia usajili wakandarasi huwa ya mwisho kabisa baada ya kuona mkandarasi amekuwa sugu licha ya kuonywa mara kwa mara kuhusu mwenendo wake kwenye utekelezaji wa miradi.
Aliyasema hayo juzi wakati wa ufungaji wa mafunzo ya siku tatu kuhusu usimamizi wa miradi kwa wakandarasi wazalendo.
“CRB ikiona mwenendo mbaya wa mkandarasi tunamwita na kuzungumza naye kujaribu kumrekebisha, lakini ikionekana ameshindikana kabisa tunamfuta na hawezi tena kufanyakazi za ukandarasi nchini.”
“Kuna ambao wanajirekebisha na tukijiridhisha tunampa usajili na anaendelea na kazi, lakini akionekana ameshindikana tunamfuta kabisa,” alisema.
Nkori aliwaka wakandarasi nchini kusoma mikataba kwa makini kabla ya kusaini ili wasije kukimbia kazi kwa kubanwa na vifungu vilivyomo wanayoingia na wateja wao.
Alisema uzoefu unaonesha baadhi ya wakandarasi wanapoona fedha nyingi kwenye mikataba wanakimbilia kusaini bila kujua athari zitakazowakuta iwapo watashindwa kutekeleza yaliyomo kwenye mikataba na wateja wao.
“Kuna mwingine akishasaini mkataba anautupilia mbali, lakini niwaambie kila mara unapaswa kuangalia mkataba unasemaje, ukikwama kitu rudi kwenye mkataba angalia athari utakazopata kisha endelea na kazi. Wengine mnakimbia kazi na mkikutana na watu mnaogopa mnadhani mnatafutwa na polisi.”
“Ni heri ukae bila kuwa na kazi kwa muda mrefu kuliko kulazimisha kazi ambayo itakufanya kuwa mtumwa. Unaonekana uko ‘site’ lakini unaishi kwa tabu mpaka unahama nyumbani kwako, sasa shida yote hii ya nini,” alihoji.
Mkurugenzi wa kampuni ya Florida Women Empowerment, Theresia Komba aliiomba serikali kuwawezesha wakandarasi wanawake ambao hawana uzoefu wa kufanya miradi na kuwapa miradi kama sehemu ya kuwajengea uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa.
Alisema wakandarasi wengi wanawake wanakosa miradi kwa kigezo cha kutokuwa na uzoefu, hivyo wakiwezeshwa kwa kupewa miradi ya kuwajengea uwezo watapata fursa ya kukua na kuwa na kampuni kubwa.
Komba alisema pia serikali na taasisi za kifedha zinapaswa kuwapa kipaumbele wakandarasi wanawake kwa kuwapa mikopo ya kufanyia miradi ya ujenzi wanapoenda kuomba mikopo.
“Mitaji ni changamoto kwetu wakandarasi wanawake, lakini kama taasisi za fedha zikitupa kipaumbele na kutupa mikopo kila tunapopata kazi tunaweza kufanya mambo makubwa na uzoefu tutapata kama tutakuwa na miradi ya kufanya watuamini tunaweza,” alisema.