Waendesha mashtaka wa Ujerumani wamemtuhumu mwanaume raia wa Gambia kwa kushiriki katika mauaji ya wapinzani wakati wa utawala wa rais wa zamani wa Gambia Yahya Jammeh.
Mshukiwa huyo anadaiwa kuwa ndiye alikuwa anawaendesha wanachama wa kikosi cha wanamgambo kwenda maeno ya kufanyia mauaji.
Waendesha mashtaka wa shirikisho wamesema jana Alhamisi kwamba wamefungua mashtaka. Uhalifu anaodaiwa kufanyika ulikuwa kuanzia mwaka 2003 hadi 2006, na vikosi vilivyotumwa na Jammeh kuzima upinzani dhidi ya utawala wake.
Mwanaume huyo alikamatwa katika mji wa kaskazini-kati wa Ujerumani wa Hannover, Machi mwaka jana.
Anaaminika kuwa alishiriki katika mauaji ya mwanadishi habari aliyekuwa mkosoaji wa serikali, na alieshukiwa kuwa hasimu wa rais. Wanaharakati wanadai kuwa alikuwa mwanachama wa kundi la "Junglers", ambalo lilikuwa kikosi cha mauaji kilichomuunga mkono Jammeh.