YANGA inazidi kupasua anga ikionyesha inalitaka kombe na wakati mbio hizo zikiendelea kocha wao Nesreddine Nabi ameshusha mkwara mzito akiwachonganisha mastaa wake wakiwamo Saido Ntizbazonkiza, Fiston Mayele, Djigui Diarra, Khalid Aucho, Fei Toto na wengine kwamba hakuna mwenye uhakika wa namba kikosini, isipokuwa kwa yule tu anayefanya makubwa tu kushinda wenzake.
Vinara hao wa Ligi Kuu Bara wakikusanya jumla ya pointi 42 katika mechi zao 16 za msimu huu, wakiwa pia ndio timu pekee ambayo haijapoteza mechi yoyote hadi sasa, wanatarajiwa kuondoka kwenda jijini Mwanza kuwahi pambano lao la ligi hiyo dhidi ya Geita Gold litakalopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Jumapili hii, lakini kabla ya safari hiyo itakayofanyika kesho Ijumaa, Kocha Nabi aliamua kufunguka mambo kadhaa ikiwamo vita ya namba kwa vijana wake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nabi alisema wakati wakiifuata Geita Gold wikiendi hii kuna mastaa wake kama wawili au watatu wanarejea katika kikosi chake ambao wanakuja kuleta vita mpya ya nafasi.
Nabi alisema beki wake wa kati Dockson Job aliyesimamishwa mechi tatu anarejea kazini akiwa hana majeraha, kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ naye anarudi kazini kufuatia kuukosa mchezo uliopita kwa kuwa na kadi tatu za njano huku pia winga Chico Ushindi akirudi kazini baada ya kupona majeraha.
Nabi alisema wakati wachezaji hao wakirejea wanakutana na wengine ambao walikuwa wanacheza huku nao wakionyesha ubora mkubwa kwa kikosi chao kusimama imara katika mechi zilizopita ambapo sasa wanatakiwa kupambana kila mmoja kuwania nafasi upya.
“Wapo wachezaji ambao wanarejea tunaweza kuwa nao katika mechi ijayo ambao wana ubora mkubwa lakini shida wanakuja kukutana na wenzao ambao katika kipindi hiki wamekuwa wakifanya makubwa,” alisema Nabi na kuongeza;