Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba, amesema zaidi ya watu 20,000 kutoka mataifa 52 duniani, tayari wamejiandikisha kupambana dhidi ya Urusi kwenye vita vinavyoendelea sasa.
Kwa mujibu wa waziri huyo wa mambo ya kigeni, watu hao watahudumu kupitia kikosi maalum cha kimataifa, licha ya kutotaja idadi kamili ambao tayari wameshawasili nchini Ukraine. Kwenye tangazo la usiku wa kuamkia leo kupitia televisheni, Kuleba alisema kwamba dunia nzima inawaunga mkono sio kwa maneno matupu, bali kwa vitendo.
Hata hivyo, hakutaja majina ya nchi wanazotoka wanajeshi hao wa kujitolea, akisema kuwa baadhi yake zinawakataza raia wao kupigana kwa ajili ya nchi nyengine. Waziri huyo amewataka pia raia wa Ukraine wanaoishi nje kuanza kampeni ya kushinikiza uwanachama wa nchi yao kwa Umoja wa Ulaya.