Subscribe Us

Header Ads

Mwalimu matatani akidaiwa kuua kwa adhabu ya viboko



Mwanafuzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Makojo Wilayani Musoma vijijini, Baraka Eliabu (18), amefariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa kwenye Zahanati ya kijiji cha Chitare alikopelekwa kwa matibabu baada ya kudaiwa kuzimia alipokuwa akiadhibiwa na mwalimu wake.


Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Ijumaa, Machi 4, 2022, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Longinus Tibushubwamu amesema tukio hilo lilitokea Machi Mosi, 2022 mchana.


Kamanda huyo amedai siku ya tukio, mwalimu aliyekuwa akifundisha somo la Jiografia darasani kwao aliyemtaja kwa jina la Jumanne Kalamu (33), aliamua kuwaadhibu wanafunzi ambao hawakufanya zoezi alilolitoa siku moja kabla na Baraka alikuwa  miongini mwa wanafunzi waliotakiwa kuadhibiwa.


Amedai baada ya mwalimu Kalamu kuwatambua wanafunzi ambao hawakufanya zoezi hilo, alianza kutoa adhabu kwa kuwachapa viboko viwili kila mmoja kwenye kiganjani.


“Walipangwa mstari na mwalimu alipomfikia Baraka na kumchapa viboko viwili alidondoka chini na kupoteza fahamu hapo hapo kisha akakimbizwa katika zahanati ya Chitare kwa ajili ya kupatiwa matibabu," amesema kamanda Tibushubwamu.


Amesema baada ya kufikishwa zahanati, mwanafunzi huyo alifariki dunia wakati akipatiwa huduma na kwamba, kutokana na tukio hilo, jeshi hilo limechukua sampuli mbalimbali za viungo vyake na kuvipeleka kwa mkemia mkuu kwa ajili ya uchunguzi zaidi.


Kamanda Tibushubwamu amedai baada ya tukio hilo, mwalimu Kalamu alijaribu kutoroka lakini baadaye alijisalimisha mwenyewe kituo cha Polisi cha Musoma Mjini na kwa sasa anashikiliwa kwa mahojiano na uchunguzi zaidi.


"Nadhani ali panic ndiyo maana akajaribu kutoroka lakini jana alikuja mwenyewe pale Central na kujitambulisha kuwa yeye ni mwalimu anayetuhumiwa kwa mauaji ya mwanafunzi kule Makojo," amesema Kamanda huyo.


Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule  amesema tayari mwili wa mwanafunzi huyo umezikwa kijijini kwao Makojo na taratibu zingine zinaendelea chini  ya jeshi la polisi.


"Uchunguzi ulifanyika na polisi wakaruhusu mwili uzikwe japokuwa mwalimu alijaribu kutoroka yeye na familia yake lakini tayari yupo mikononi mwa jeshi la polisi,” amesema Dk Haule.