Subscribe Us

Header Ads

IMF Yataka Umakini Athari Vita Ukraine



MAMLAKA za Fedha zimetakiwa kufuatilia kwa makini mwenendo wa kupanda kwa bei kimataifa kwa kuzingatia mfumuko wa bei wa ndani ili kurekebisha hali hiyo.


Hayo yalibainishwa na Bodi ya Utendaji ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) katika taarifa yao kwa umma.


Bodi hiyo iliyoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Kristalina Georgieva, ilikutana Machi 4 mwaka huu kujadili athari za kiuchumi za vita kati ya Ukraine na Urusi na uwezekano wa msaada wa haraka wa kifedha kwa nchi athirika.


Kwa mujibu wa IMF, athari za kiuchumi kutokana na vita hiyo tayari ni kubwa kwa sababu bei za nishati na bidhaa ikiwemo ngano na nafaka nyingine zimepanda na kuongeza shinikizo la mfumuko wa bei kutokana na kukatika kwa ugavi na kurudishwa nyuma na Covid-19.


“Athari za kutikiswa kwa bei zitakuwa kwa dunia nzima hasa kwa kaya maskini ambazo chakula na mafuta vimepanda. Ikiwa mzozo huu utaendelea, uharibifu wa kiuchumi utakuwa mkubwa zaidi na vikwazo dhidi ya Urusi navyo vitakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa dunia na masoko ya fedha na kuenea kwenye nchi nyingine,” ilisema IMF.


Iliongeza: “Mamlaka za Fedha zinahitaji kufuatilia kwa makini mwenendo wa kupanda kwa bei kimataifa kwa kuzingatia mfumuko wa bei wa ndani ili kurekebisha hali hiyo. Sera ya fedha itahitaji kusaidia kaya zilizo hatarini zaidi kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha.”


Ilisema mgogoro huo pia utasababisha changamoto ya mabadiliko ya kisera na kusababisha ugumu zaidi wa mazingira ya kisera kadri uchumi wa dunia unvyoimarika kutoka katika janga la Covid-19 na kuongeza kuwa licha ya athari za kibinadamu, athari za kiuchumi tayari ziko dhahiri nchini Ukraine kutokana na bandari na viwanja vya ndege kufungwa na kuharibiwa, barabara na madaraja nayo yameharibiwa.


IMF ilibainisha kuwa ingawa ni vigumu kutathmini mahitaji ya kifedha kwa sasa, ni dhahiri kwamba Ukraine tayari imeshaomba msaada wa kifedha wa dharura wa Dola bilioni 1.4 chini ya Chombo cha Ufadhili wa haraka cha IMF.


Pia ilisema vikwazo vilivyotangazwa dhidi ya Benki Kuu ya Shirikisho la Urusi vitaifanya isiweze kupata huduma ya kifedha ya kimataifa kwa ajili ya kusaidia sarafu yake na mfumo wake wa kifedha.


“Vikwazo vya kimataifa kwa mfumo wa kibenki wa Urusi na kutengwa kwa mabenki yake katika Mfumo wa Malipo wa Kimtaifa (SWIFT) kumevuruga uwezo wa Urusi kupokea malipo ya mauzo ya nje, kulipia bidhaa kutoka nje na kushiriki katika shughuli za kifedha za mipakani. Ingawa ni mapema kutabiri athari kamili ya vikwazo hivi, tayari tumeona kushuka kwa kasi kwa bei za mali pamoja na kiwango cha ubadilishaji wa fedha ya Urusi (Ruble).


“Nchi ambazo zina uhusiano wa karibu wa kiuchumi na Ukraine na Urusi ziko katika hatari fulani ya uhaba na usumbufu wa usambazaji na zinaathirika zaidi na ongezeko la wakimbizi,” ilisema IMF.


Kwa mujibu wa IMF, vita vinavyoendelea na vikwazo husika pia vitakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa dunia.


Wakati akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Channel Ten hivi karibuni, Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Haji Semboja, alizitaja athari tatu za kiuchumi zinazoweza kujitokeza katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania kutokana na vita hivyo.


“Athari tunazo za aina nyingi, kwa sasa tunazungumzia athari za muda mfupi zitakazojitokeza na kwa sababu tunaizungumzia


Tanzania ambayo ipo Afrika, sisi ni waagizaji wa mafuta, nishati ambayo inaendesha magari yetu na kwenye masuala ya umeme na mitambo mingine.


Kwa hiyo tunachokitegemea kwa haraka ni kwamba


kutakuwa na mabadiliko ya bei za mafuta kupanda,” alisema.


Profesa Semboja alisema vita hivyo si vita inayohusu masuala ya kupigana tu ila pia ya kiuchumi kwa sababu nchi za magharibi zimeiwekea vikwazo Urusi katika mambo mbalimbali yakiwemo masoko ya kifedha.