Mamlaka nchini Benin imemwachilia huru kiongozi wa Nigeria anayetaka kujitenga, Sunday "Igboho" Adeyemo, kulingana na msemaji wake.
Bw Igboho alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Benin Julai 2021 pamoja na mkewe kwa ombi la Nigeria, ingawa mkewe aliachiliwa siku chache baadaye. Wanandoa hao walisemekana kuelekea Ujerumani ambako mkewe ni raia.
Alishtakiwa kwa kuingia Benin kinyume cha sheria na kupanga kuleta fujo lakini alikanusha mashtaka. Mamlaka ya Nigeria haikuwahi kutoa ombi rasmi la kurejeshwa kwake nchini mwake.
Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, msemaji wake alisema Bw Igboho aliachiliwa kwa kiongozi wa shirika mwamvuli la Makundi ya Kujitawala ya Yoruba, Banji Akintoye.
Maelezo juu ya kuachiliwa kwake bado hajayatolewa
Nigeria inamtuhumu Bw Igboho kwa kuhifadhi silaha, akitaka nchi hiyo isambaratike na kuchochea mauaji ya kikabila.
Bw Igboho anasifiwa kama shujaa na wafuasi wake baada ya kutoa wito kwa taifa la Yoruba kusini-magharibi mwa nchi hiyo.
Alitoroka nchini baada ya kuvamiwa nyumbani kwake na polisi wa siri wa Nigeria mnamo Julai 2021 ambapo washirika wake wawili waliuawa.