Subscribe Us

Header Ads

Askofu Bagonza, Sheikh Kabeke wampongeza Samia kuachiwa Mbowe

 



Askofu  wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia uamuzi wa Jamhuri kufuata kesi ya tuhuma za  ugaidi iliyokuwa ikimkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.


Akizungumza kwa simu Mwananchi Digital, Dk Bagonza amesema uamuzi wa kuifuta kesi ni mzuri, licha ya kuwa umechelewa kuchukuliwa.


“Nampongeza Rais Samia kwa hatua aliyochukua; ni hatua muhimu iliyochukuliwa kwa kuchelewa. Sijui kama amefanyia kazi maombi na ushauri wetu viongozi wa dini. Lakini jambo muhimu ni kwamba nampongeza kwa hatua aliyochukua,” amesema Dk Bagonza.


Sheikh wa Mkoa wa Mwanza,  Hassan Kabeke ameungana na Askofu Bagonza kumpongeza Rais Samia kwa kuwasikiliza na kufanyia kazi ombi na ushauri wa viongozi wa dini kuhusu kesi ya Mbowe na wenzake.


“Hili la Mbowe na wenzake kuachiwa huru ni la shukurani na pongezi kwa viongozi wa dini waliowasilisha ombi na ushauri kwa Rais Samia wa busara na hekima kutumika kumaliza kesi hiyo. Nampongeza na kumshukuru pia Rais Samia kwa kusikiliza na kufanyia kazi ombi na ushauri wa viongozi wa dini,” amesema Sheikh Kabeke


Amesema tofauti na ombi la Mbowe na wenzake kuachiwa huru lililowasilishwa mbele ya Rais na kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ombi na ushauri wa viongozi wa dini ulipokelewa vema kwa sababu ya imani na utii wa umma kwa viongozi hao wa kiroho.


“Ombi la Mbowe na wenzake kuachiwa huru lilipotolewa na Zitto na hata Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu lilipokelewa kwa mitazamo tofauti na watu; lakini lilipotolewa na viongozi wa dini kwa nafasi yao ya ulezi wa kiroho busara na hekima imetumika,” amesema Sheikh Kabeke


Akifafanua, kiongozi huyo wa dini amesema japo suala hilo lilikuwa ni la kisheria, lakini matumizi ya sheria lazima yaambatane na hekima na busara kama walivyoshauri viongozi wa dini walipokutana na Rais Samia.


“Mbowe na wenzake kuachiwa huru ni ishara ya kutumika kwa busara na hekima. Ni jambo la kuwapongeza viongozi wa dini kwa ushauri waoa; lakini pia Rais Samia kwa kuwa kiongozi msikivu,” amesema.


Wakati huohuo Askofu  Bagonza, amemshauri Mbowe kutulia, kutafakari na kusonga mbele na kuangalia maisha yake ya kawaida na ya kisiasa.


“Kwanza nampa Mbowe na wenzake pole kwa yaliyowakuta; muhimu nataka kumweleza kuwa bado anayo nafasi ya kufanya siasa,” amesema Dk Bagonza ambaye ni miongoni mwa viongozi wa dini waliowasilisha ombi na ushauri kwa Rais ili mamlaka husika katika kesi hiyo kutumia busara kumaliza suala hilo la Mbowe na wenzake.