Subscribe Us

Header Ads

Tanzania yaondoa tozo ya mafuta kwa kila lita


Wizara ya nishati nchini Tanzania imefikia uamuzi wa kuondoa tozo ya shilingi 100 kwa kila lita ya Dizeli, Petroli na mafuta ya taa.

Tozo hiyo ilipaswa kulipwa na watumiaji wa mafuta nchini humo kuanzia mwezi Machi mpaka Mei , mwaka huu huku taifa hilo likiendelea kutathmini mwenendo wa soko la dunia katika mafuta.

Hatua hii itapelekea serikali kupunguza mapato ya shilingi bilioni 30 za Tanzania kwa kila mwezi.

Aidha uamuzi huo umekuja kutokana na kupanda bei za mafuta katika soko la dunia kunakosababishwa na vita kati ya Urusi na Ukraine.

Uamuzi huu pia unaenda sambamba na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa ya kupunguzwa kwa tozo zinazotozwa na taasisi mbalimbali katika bidhaa za mafuta hapa nchini zenye thamani ya Sh102 bilioni kwa mwaka, kwa lengo la kupunguza bei za mafuta na kuwapa unafuu wananchi.

Taasisi zinazoguswa na maelekezo hayo ya Rais Samia ni, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (tozo ya udhibiti), Mamlaka ya Bandari (tozo ya miundombinu), Mamala ya Mapato Tanzania (tozo ya kuchakata taarifa), Shirika la Viwango Tanzania (tozo ya kupima ubora wa mafuta kwenye meli na gharama ya uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta).

Hata hivyo bei mpya ya mafuta itaanza kutumika Machi 02, 2022 zikizingatia marekebisho ya kanuni alizoweka waziri wa nishati, January Makamba.