Subscribe Us

Header Ads

Radi Yaua Saba, Ng’ombe Sita



WATU saba, wakazi wa kijiji cha Milundikwa, Kata ya Nkandasi katika wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa wamefariki dunia na wengine zaidi ya 10 kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi wakiwa shambani.


Pia ng'ombe sita wamekufa baada ya kupigwa na radi hiyo wakiwa malishoni.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, William Mwampaghale alithibitisha kutokea kwa mkasa huo ulisababisha taharuki kijijini humo.


Alisema majeruhi walikimbizwa katika zahanati ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Milundikwa kwa matibabu.


Kamanda Mwampaghale awali alitaja majina ya watu watano kuwa ndio wamekufa lakini wakati tunakwenda mitamboni, akatoa taarifa kwamba watu wengine wawili miongoni mwa majeruhi 14 aliowataja awali pia wamefariki dunia na kufanya idadi kufika saba. Hata hivyo, alisema hakupata majina ya hao wawili walioongezeka.


Majina ya watano aliowataja awali ni Yusuph Mbalamwezi (24), Leonard Francisco Wayomba (21), Fadhili Wayomba (24), Shukuru Mutayagwa (28) na Abinet Kazumba (8).


Majeruhi waliotajwa awali na Kamanda Mwampaghale ambao miongoni mwao wawili walifariki dunia wakati tunakwenda mitamboni ni Veronica Saanane (27), Fobi Mbonile (28, Solostina Sokoni (39), Edina Noel (39), Getruda Mwananjela (34), Tatu Miyula (10), Teddy Wazamani (37), Mary Kauzeni (18), Daniel Kamilembe (19) na Lenatha Chakula (51)


Wengine waliojeruhiwa ni Margaret Xavery (40), Leticia Fataki (38) na Veronica Swaila (27).


Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Mtendaji Kata ya Nkandasi, Given Kisantola alisema lilitokea juzi saa tisa alasiri.


"Mvua ilipoanza kunyesha watu hao wakiwa shambani wakipanda maharage ndipo walipokimbilia kwenye nyumba ndogo ya shambani kujikinga. Ghafla radi ikapiga na kusababisha maafa hayo," alisema.


Diwani wa Kata ya Nkandasi, Mpemba Evarist alisema marehemu hao pamoja na majeruhi walikuwa wakipanda maharage kwenye shamba kama vibarua na kuwa majanga hayo yaliwakuta walipokimblia kwenye nyumba ndogo ya shambani ili kujikinga na mvua