MAWAZIRI kutoka nchi sita wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanadaiwa kukwamisha vikao vya Bunge la jumuiya hiyo (EALA) jijini Arusha.
Wabunge wa bunge hilo wamedai kuwa hawawezi kuendelea na vikao kwa kuwa rasimu zilizokuwa ziwasilishwe bungeni zimekosa uwakilishi wa mawaziri au wawakilishi wao.
Mbunge kutoka Kenya, Kenneth Kilonzo Muthioka alidai kuwa kukosekana mawaziri katika vikao vya EALA kunasababisha malengo ya bunge hilo kutotimia kwa wakati.
Alitoa mfano wa ripoti iliyokuwa iwasilishwe wiki iliyopita kuhusu gharama za usafiri wa ndege kwa wananchi wa nchi za EAC kwa kuwa ni kubwa na zinahitaji majibu ya mawaziri hao.
"Kwa mfano, gharama za kutoka Nairobi kwenda Arusha kwa ndege ni ghali zaidi kuliko kutoka Nairobi kwenda Dubai," alisema Muthioka.
Mbunge kutoka Tanzania, Mariam Ussi Yahaya alisema wabunge walikuwa wajadili ripoti nne zikiwemo mbili zilizokuwa ziwasilishwe na mawaziri na moja ni ripoti ya kamati ya hesabu lakini haikuwa hivyo kwa sababu ya mawaziri hawakuhudhuria vikao.
Mariam alisema moja ya ripoti zilizokuwa zijadiliwe inahusu sheria za EAC ambazo zinastahiil zianze pia kutumika kwenye nchi wanachama.
"Hoja nyingine zilizokuwa zijadiliwe ni muswada wa usafiri wa anga kwa kutumia ndege (cassoa) ambao imeonekana kuwa ni usafiri ghali zaidi kwa nchi za jumuiya hiyo na hivyo kuwaumiza wananchi wetu ambao wamekuwa wakisafiri kufanya biashara na wanafunzi kwenda kusoma kwenye nchi wanachama," alisema.
Mariam alisema ripoti inaonesha kuwa usafiri ndani ya nchi wanachama wa EAC ni ghali hivyo ni muhimu jambo hilo lijadiliwe ili mawaziri waone namna ya kupunguza gharama za usafiri wa anga.
"Wabunge tunapaswa tufanye jambo ili wananchi wetu wanufaike na Jumuiya yao ya Afrika Mashariki kwa gharama nafuu za usafiri, ndio maana tulijiuanga kuwaomba mawaziri waone namna ya kupunguza gharama za anga kwa nchi za EAC," alisema.
Spika wa Muda wa bunge hilo, Abdulkadir Aden aliahirisha bunge hilo hadi kesho.
Waziri mteule, Betty Maina kutoka Kenya anatarajiwa kuapishwa ili awe miongoni mwa mawaziri wa EAC baada ya waziri aliyekuwepo, Aden Mohamed kujizulu kutokana na masuala ya uchaguzi nchini kwao.