Kumekucha sasa nchini Ukraine, na jua linachomoza huku milio ya hatari ikiendelea kurindima katika anga ya Kyiv, ikiwa ni siku ya tano ya uvamizi leo. Wakazi wengi wa mji huo wameendelea kujificha na kujihifadhi chini ya ardhi.
Milipuko zaidi imeripotiwa usiku wa kuamkia leo katika mji mkuu wa Ukraine na miji mingine nchini humo.
Ukraine inadai kuwa vikosi vyake vilifanikiwa kuzuia mashambulizi kadhaa yaliyofanywa na wanajeshi wa Urusi waliokuwa wakijaribu kuvamia viunga vya mji mkuu.
"Tulionyesha kwamba tunaweza kulinda nyumba yetu dhidi ya wageni wasioalikwa," alisema Kamanda wa Jeshi Kanali Jenerali Alexander Syrsky katika taarifa iliyotolewa muda mfupi uliopita.
Wakati huo huo video moja ilichapishwa kwenye mitandao usiku ikionyesha mashambulizi yanaodaiwa kufanywa na makombora ya Urusi yakielekezwa kwenye moja ya majengo ya makazi ya watu mjini Chernihiv, taarifa zinasema.
Milipuko pia imeripotiwa huko Kharkiv upande wa mashariki, kwenye mapigano ya jumapili baada ya majeshi ya Ukraine kurejesha mikononi mwao mji huo mkubwa wa pili wa nchi hiyo kutoka mikononi mwa Urusi.