Iran imekataa wito wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani, IAEA, linalotaka kuyakaguwa maeneo mawili, ikisema hatua hiyo itaibuwa upya mzozo baina ya pande hizo mbili.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Abbas Mousavi, amesema hivi leo kwamba endapo IAEA itaendelea na madai yake hayo itaharibu mahusiano kati ya pande hizi mbili.
Kwa zaidi ya miezi minne sasa, Iran imekuwa ikiikatalia IAEA kutembelea maeneo mawili ambayo shirika hilo linaamini kuna madini ya urani.
Wito huo wa uchunguzi uliotolewa na Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi, unaungwa mkono na Ujerumani, Uingereza na Ufaransa.
Iran inahoji kwamba madai hayo yanakiuka mipaka iliyowekewa shirika hilo kisheria, na badala yake inalituhumu kufuata shinikizo la kisiasa la mashirika ya ujasusi ya Israel.
Mkataba wa nyuklia kati ya Iran na mataifa makubwa duniani ulisainiwa Juni 2015, lakini Rais Trump wa Marekani aliiondowa nchi yake kutoka mkataba huo na kuzibakisha Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, China na Urusi.