Subscribe Us

Header Ads

Kuelekea Mechi ya KESHO...GSM Afanya Kufuru Yanga...Aweka Mezani Milioni 400 Mnyama Afe Kesho



KATIKA kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Simba, Mdhamini wa Yanga, Bilionea Gharib Said Mohammed ‘GSM’, juzi alifanya kikao kizito na wachezaji wakiongozwa na mshambuliaji hatari, Fiston Mayele.

Katika kikao hicho ambacho kilienda sambamba na kufturu pamoja, pia benchi lote la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na Kocha Mkuu, Mtunisia, Nasreddine Nabi, lilikuwepo.


Hiyo ni katika kuweka mikakati ya ushindi kuelekea mchezo wa Kariakoo Dabi utakaozikutanisha Yanga dhidi ya Simba utakaopigwa keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.


Yanga ambayo inaoongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 51, ikifanikiwa kuifunga Simba yenye pointi 41, basi watakuwa wana nafasi kubwa zaidi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, mapema.


Mmoja wa mabosi wakubwa wa Yanga, alisema GSM juzi Jumanne jioni alitoa mwaliko huo kwa wachezaji na benchi la ufundi kwa lengo kuwapa hamasa na morali ya kupata ushindi katika dabi hiyo.


Bosi huyo alisema, tukio hilo lilifanyika nyumbani kwa bilionea huyo Kigamboni, Dar es Salaam.


Aliongeza kuwa, kikao hicho kilikwenda sambamba na ahadi ya fedha kwa wachezaji bonasi ya shilingi milioni 400 kama wakifanikiwa kuwafunga Simba.


“Jana (juzi) wachezaji, benchi la ufundi na baadhi ya viongozi wa Yanga walikutana na mdhamini GSM kwa ajili kupata Iftar iliyokwenda sambamba na kikao cha kuwakumbusha malengo tuliyojiwekea msimu huu ambayo ni kuchukua makombe yote tunayosindania.


“Katika kikao hicho, GSM aliwaongezea morali wachezaji kuhakikisha wanashinda mchezo huo ambao ni muhimu kwetu kupata ushindi.


“Wachezaji wamejiapiza kupambana kwa ajili ya kupata ushindi utakaotuweka katika nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa wa ligi msimu huu,” alisema mtoa taarifa huyo.


Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Yanga, Hassani Bumbuli, kuzungumzia hilo alisema: “Ni kweli wachezaji, benchi la ufundi na baadhi ya viongozi tulipewa mwaliko na mdhamini wetu GSM nyumbani kwake kwa ajili ya kwenda kufuturu.


“Mara baada ya kufuturu yalikuwepo mazungumzo ambayo ni siri kati ya mdhamini wetu, wachezaji, benchi la ufundi na viongozi.


“Kuhusu bonasi hiyo ipo katika kila mchezo tutakaoucheza licha ya kuwepo utofauti mkubwa kwa baadhi ya michezo ambayo inaongozeka ikiwemo hii dhidi ya Simba.”